Mhubiri Mlango 12 Ecclesiastes

Mhubiri 12:1 Ecclesiastes 12:1

Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.

Mhubiri 12:2 Ecclesiastes 12:2

Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua;

Mhubiri 12:3 Ecclesiastes 12:3

Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetema; Hapo wenye nguvu watakapojiinamisha; Na wasagao kukoma kwa kuwa ni haba; Na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza;

Mhubiri 12:4 Ecclesiastes 12:4

Na milango kufungwa katika njia kuu; Sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo; Na mtu kusituka kwa sauti ya ndege; Nao binti za kuimba watapunguzwa;

Mhubiri 12:5 Ecclesiastes 12:5

Naam, wataogopa kilichoinuka Na vitisho vitakuwapo njiani; Na mlozi utachanua maua; Na panzi atakuwa ni mzigo mzito; Na pilipili hoho itapasuka; Maana mtu aiendea nyumba yake ya milele, Nao waombolezao wazunguka njiani.

Mhubiri 12:6 Ecclesiastes 12:6

Kabla haijakatika kamba ya fedha; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi kuvunjika kisimani; Au gurudumu kuvunjika birikani;

Mhubiri 12:7 Ecclesiastes 12:7

Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa.

Mhubiri 12:8 Ecclesiastes 12:8

Mhubiri asema, Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili!

Mhubiri 12:9 Ecclesiastes 12:9

Walakini, kwa sababu huyo Mhubiri alikuwa na hekima, aliendelea kuwafundisha watu maarifa, naam, akatafakari, akatafuta-tafuta, akatunga mithali nyingi.

Mhubiri 12:10 Ecclesiastes 12:10

Huyo Mhubiri akatafuta-tafuta ili apate kuona maneno yapendezayo, na yale yaliyoandikwa kwa unyofu, yaani, maneno ya kweli.

Mhubiri 12:11 Ecclesiastes 12:11

Maneno yao wenye hekima huwa mfano wa michokoo; na kama misumari iliyogongomewa sana; ndivyo yalivyo maneno yao walio wakuu wa makusanyiko, ambayo yatoka kwa mchungaji mmoja.

Mhubiri 12:12 Ecclesiastes 12:12

Tena, zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo; hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi; na kusoma sana huuchosha mwili.

Mhubiri 12:13 Ecclesiastes 12:13

Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.

Mhubiri 12:14 Ecclesiastes 12:14

Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.